Familia nne mkoani Mwanza zakosa makazi nyumba ikibomolewa
Familia nne zilizokuwa zikiishi katika nyumba moja iliyoko mtaa wa Isamilo Kaskazini 'B' kata ya Isamilo jijini Mwanza zimekosa mahala pa kuishi baada ya nyumba waliyokuwa wanaishi kubomolewa huku taarifa zikidai kwamba mmiliki wa eneo hilo alishaliuza kwa mtu mwingine anayehitaji kulibadilishia matumizi.
Familia zilizoathirika kutokana na ubomoaji huo ni
familia ya Happiness Lukenza aliyekuwa anaishi na mtoto wake mmoja, na
wapangaji watatu ambao ni David Abel mwenye mke na watoto wawili, na wanafunzi
wawili ambao ni Yassin Jafari na Enodius Eustard.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Mwenyekiti wa Mtaa
huo, Athuman Butu, eneo hilo mali ya Happiness Lukenza na mmewe (Lucas) ambaye
walitalakiana zaidi ya miaka sita iliyopita liliuzwa na familia hiyo huku
mwanamke huyo akikataa kuondoka kwenye nyumba yake kwa kile anachodai kwamba
hajaridhika na mgao wa fedha za mauzo ya nyumba hiyo.
Butu amesema kwamba nyumba hiyo ambayo tayari imebomolewa
kuwa ofisi yake ilipokea amri ya mahakama ikimtaarifu juu ya zoezi la kuwaondoa
na kuvunja nyumba hiyo jambo ambalo limetekelezwa leo mchana wa leo na mabaunsa
waliokua wamevaa fulana zenye jina la US Born Security mgongoni ambao hawakuwa
tayari kuzungumza.
Amesema baada ya kupokea barua hiyo amefika katika eneo
hilo kusimamia uvunjaji na ubomoaji sambamba na kuhakikisha hakuna uharibifu na
upotevu wa mali za wapangaji wa nyumba hiyo.
"Tulipokea wito wa kuhakikisha tunasimamia ili zoezi
la kuwaondoa linafanyika kwa amani na utulivu na tumeshuhudia zoezi la uondoaji
vitu na ubomoaji. Tumekuja kuhakikisha hakuna upotevu wa mali kwa sababu zoezi
la kuondoa mali limefanyika wakati wapangaji wengine wakiwa hawapo,"
amesema Butu
Mpangaji katika nyumba hiyo, David Abel amesema alikuwa
amelipa kodi ya miezi sita kwa ajili ya kuishi katika nyumba hiyo iliyokuwa
inafikia ukomo Novemba mwaka huu.
Abel ametoa wito kwa wamiliki wa nyumba na mahakama
inapotoa maamuzi ya migogoro inayohusisha makazi ifike na kutoa taarifa kwa
wapangaji ili kuwaepushia wapangaji usumbufu huku akisema tukio hilo limeiacha
familia yake bila mahala pa kwenda.
"Nina mke na watoto wawili ambao nilikuwa naishi nao
hapa. Asubuhi tumeamka hatujui kinachoendelea ghafla wakaja mabaunsa wakaanza
kutoa vyombo vyetu ndani na kupeleka nje wakati nimelipa kodi ya miezi sita
Sh165,000 hii siyo sawa," amesema Abel
Kwa upande wake Mwanafunzi wa Chuo Cha Mwanza Drive
kilichopo jijini hapa, Yassin Jafari amesema amehamia katika nyumba hiyo siku
tatu zilizopita na kumlipa Happiness Lukenza Sh75,000 ikiwa ni kodi ya miezi
mitatu.
Juhudi za kumpata, Happiness Lukenza ambaye alikuwa
mmiliki wa eneo hilo kabla halijauzwa zimegonga mwamba kutokana na kutokuwa
katika eneo hilo huku simu yake ikiita bila kupokelewa na taarifa zikidai
kwamba anafuatilia barua ya kusitisha ubomoaji huo katika mahakama ya rufaa
iliyoko mkoani hapa.
No comments
Post a Comment