Jeshi la polisi Mwanza lanasa jezi feki za Simba na Yanga
Jeshi
la Polisi Mkoa wa Mwanza limekamata jezi feki dazani 296 za Simba na Yanga
jijini hapa zikiuzwa na wafanyabiashara huku wito ukitolewa kwa
wauzaji kuuza bidhaa halali ili kutohujumu mapato ya klabu hizo.
Akizungumza
katika mkutano na waandishi wa habari jijini Mwanza leo, Kamanda wa Polisi
mkoani hapa, Ramadhan Ng'anzi amemtaja aliyekamatwa na bidhaa hizo ni
mfanyabiashara, Said Furaha (31) mkazi wa Nundu.
Amesema mtuhumiwa huyo alikamatwa Julai 5 saa 12:30 mchana eneo la barabara ya Pamba sokoni wilaya ya Nyamagana kwa kosa la kupatikana na jezi bandia dazani 145 zenye nembo ya klabu ya Simba zinazomilikiwa na Kampuni ya Vunjabei na jezi dazani 151 zenye nembo ya Yanga zinazomilikiwa na Kampuni ya GSM, kitendo ambacho ni kinyume cha sheria.
Kamanda
Ng'anzi amesema kuwa jeshi lake lilipata taarifa kutoka kwa maafisa masoko wa
kampuni hizo kuwa jijini Mwanza kuna mfanyabiashara anaesambaza na kuiza jezi
bandia ndipo ufuatiliaji wa kina na haraka ulifanyika na kufanikiwa kumkamata
mtuhumiwa akiwa na jumla ya dazani 296 bandia za klabu hizo dukani kwake.
"Jeshi letu
linaendelea na upelelezi wa kina kuhusiana na shauri hili ili kubaini mtandao
mzima wa wahusika wote wanaotengeneza, kuagiza na kuingiza nchini bidhaa hizo
bandia, ambapo inapelekea wadhamini wa klabu hizo kukosa mapato,"
"Upelelezi wa shauri hili unakamilishwa mara moja na mtuhumiwa atafikishwa mahakamani haraka iwezekanavyo," amesema Ng'anzi.
Kwa upande wake,
Mshauri wa kampuni ya GSM tawi la Mwanza, Mahsen Omar ameomba mamlaka
kuhakikisha watuhumiwa wanafikishwa kwenye vyombo vya sheria ili kukomesha
tabia hizo.
"Tumekamata jezi
feki baada ya kufanya msako tunaomba hili jambo lisiishie hapa tuone hatua
zikichukuliwa, biashara hii inapoteza mapoteza ya klabu na wadhamini
wake," amesema.
Meneja wa Vunjabei Kanda ya Ziwa, Said Malekela amelishukuru jeshi la polisi na kuomba hatua zaidi kuendelea kuchukuliwa huku akiwataka mashabiki wanaonunua jezi za klabu ya Simba kutambua bidhaa halali zenye nembo ya timu hiyo na ile ya Vunjabei.
No comments
Post a Comment