Mahakama yahairisha hukumu ya akina mdee na wenzake
Mahakama Kuu ya Tanzania imeahirisha kutoa uamuzi wa
maombi ya Halima Mdee na wenzake 18 ya kutaka kibali cha kufungua kesi ya
kupinga kuvuliwa uanachama na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) hadi
Ijumaa ya Julai 8, 2022.
Uamuzi huo ulikuwa utolewe leo Jumatano Julai 6, 2022 na
Jaji Mustapha Ismail lakini Naibu Msajili wa Mahakama hiyo, Elimo Massawe
amesema, haujakamilika na utatolewa Ijumaa hii.
Uamuzi huo unatarajia kutoa hatima ya safari yao ya
kupigania uanachama wao na kulinda ubunge wao.
Mdee na wenzake wanaomba ridhaa ya kupinga uamuzi wa
Baraza Kuu la Chadema wa Mei 11, 2022 kwa utaratibu wa Mapitio ya Mahakama,
yaani ipitie uamuzi wa Chadema kisha itoe amri mbili.
Pia, wanataka Mahakama itengue uamuzi wa Chadema kuwavua
uanachama kwa madai hawakupewa haki ya kusikilizwa kabla ya kuvuliwa uanachama.
Novemba 27, 2020 Kamati Kuu ya Chadema iliwatia hatiani
kwa kosa la kwenda kuapishwa kuwa wabunge wa viti maalumu bila ridhaa ya chama.
Mapambano ya Mdee na wenzake yalianza rasmi mahakamani
Mei 12, 2022, walipowasilisha mahakamani maombi yao ya ridhaa.
Pia, walifungua maombi ya zuio la muda ili kulinda ubunge
hadi maombi yao ya ridhaa ya kufungua maombi ya kupinga kuvuliwa uanachama
yatakaposikilizwa na kuamuliwa.
Lengo la maombi hayo lilikuwa kumzuia Spika wa Bunge na
Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) kutekeleza uamuzi huo wa Chadema, yaani
wasitangaze nafasi zao ziko wazi.
Mbali na Bodi ya Wadhamini wa Chadema, wajibu maombi
wengine ni NEC na Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG).
Maombi hayo yalitajwa Mei 16, mwaka huu na Mahakama
ikapanga kusikiliza maombi ya zuio Juni 13.
Mawakili wao ni Aliko Mwamanenge, Ipilinga Panya, Edson
Kilatu na Emmanuel Ukash ambao waliomba Mahakama iamuru kina Mdee waendelee na
ubunge hadi hapo itakapoamua vinginevyo.
Mawakili wa Chadema, Peter Kibatala na Jeremiah Mtobesya
walipinga kutolewa kwa amri hiyo wakiainisha kasoro za kisheria katika maombi
hayo.
Jaji John Mgetta aliridhia maombi ya mawakili wa kina
Mdee na kutoa amri waendelee na ubunge wao mpaka maombi hayo ya zuio
yatakaposikilizwa.
Juni 22, 2022, Jaji John Mgetta alitupilia mbali maombi
ya kina Mdee baada ya kukubaliana na mawakili wa Chadema kuwa yalikuwa na
kasoro za kisheria.
Jaji Mgetta alikubali kuwa katika sehemu ya uthibitisho,
walithibitisha taarifa zilizomo katika hati ya kiapo badala ya hati ya maelezo
na kukosea jina la mjibu maombi wa kwanza.
Jaji alikubali katika maombi yao, kina Mdee waliitaja
Bodi ya Chadema kama ‘The Board of Trustee of Chama cha Demokrasia na Maendeleo
(Chadema)’, badala ya The ‘Registered Trustee’ of Chama cha Demokrasia na
Maendeleo (Chadema). Kina Mdee hawakupoteza muda, Juni 23 walifungua upya
maombi hayo baada ya kurekebisha kasoro.
Mawakili wa Chadema waliibua pingamizi dhidi ya maombi
hayo ya zuio na Jaji Ismail akapanga kusikiliza pingamizi hilo Juni 29 mchana.
Pia, Jaji Ismail alitoa amri ya kulinda ubunge wa kina
Mdee hadi siku ya usikilizwaji wa pingamizi la Chadema.
Serikali haikuwasilisha kiapo kinzani; na Chadema
iliwasilisha kiapo kinzani dhidi ya maombi yote ya ridhaa na ya zuio, lakini
nje ya muda walioamuriwa na Mahakama.
Badala ya Juni 28, wao waliwasilisha Juni 29 asubuhi,
huku wakiwa wameibua pingamizi dhidi maombi ya ridhaa.
Wakati huohuo, mawakili wa kina Mdee waliandaa
mapingamiizi ya awali dhidi ya viapo kinzani vya Chadema, wakidai kuwa kiapo
kinzani dhidi ya maombi ya zuio, kimewasilishwa nje ya muda.
No comments
Post a Comment