Mkurugenzi mpya TPA apewa wiki mbili bandari ya Bagamoyo
Naibu Waziri wa
Uchukuzi, Atupele Mwakibete, ametoa siku Kumi na Nne (14), kwa Mkurugenzi Mkuu
wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA) kuwasilisha ripoti ya vitu
vyote muhimu vinavyohitajika kwa maboresho ya miundombinu katika Bandari ya Bagamoyo.
Meneja Miliki wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA), Alexander Ndibalema, akimuonesha Naibu Waziri wa Uchukuzi, Atupeleke Mwakibete (mwenye koti la Buluu), eneo lililotengwa kwa ajili ya Ujenzi wa Bandari ya Mbegani, wakati Naibu Waziri alipotembelea eneo hilo, wilayani Bagamoyo mkoani Pwani.
Akizungumza mara
baada ya kukagua Bandari hiyo mkoani Pwani, Naibu Waziri Mwakibete, amesema
kuboreshwa kwa Bandari hiyo kutarahisha shughuli za utalii nchini na hivyo
kukuza pato la wananchi wa mkoa huo na Taifa kwa ujumla.
“Kwa kuwa eneo
hili la Bagamoyo ni muhimu sana kwa utalii nampa Mkurugenzi Mkuu wa TPA wiki
mbili alete watalaam hapa waangalie vitu muhimu vya kuboresha”, amesisitiza
Naibu Waziri Mwakibete.
Naibu Waziri
Mwakibete amesema pamoja na maboresho ambayo Serikali imejipanga kuyafanya kwa
Bandari bado inaendelea na mkakati wake wa kurasimisha Bandari bubu
zinazozunguka eneo la Bahari ya Hindi ili kuweza kupunguza biashara za magendo
ambazo zimekuwa zikiendelea kufanyika bila usimamizi mzuri.
Naye, Meneja
Miliki wa TPA, Ndibalema Alexander, amemuhakikishia Naibu Waziri Mwakibete kuwa
TPA iko tayari na itatuma watalaam wa kufanya tathmini ya mahitaji halisi ya
maboresho ya miundombinu ya Bandari hiyo lengo likiwa ni kuongeza wigo wa
mapato kwa Mamlaka na kuhakikisha wananchi wanapata huduma katika miundombinu
bora.
Kwa upande wake
Mwenyekiti wa Halmashauri ya Chalinze, Hassani Rajabu, ameishukuru Serikali kwa
kutupia jicho Bandari ya Bagamoyo na kusema maboresho ya miundombinu
yatakayofanywa na Serikali inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan, itaongeza
pato kwa kuwa itaongeza idadi ya watalii wanaotembelea vivutio mbalimbali
vilivyopo mkoani Pwani.
Naibu Waziri
Mwakibete yuko mkoani Pwani kwa ziara ya kikazi ya siku mbili ya kukagua miradi
mbalimbali inayosimamiwa na Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi.
Mkurugenzi wa Halmashauri ya Bagamoyo, Shauri Selenda, akifafanua kwa Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mashimba Ndaki, kuhusu utendaji wa soko la Bagamoyo, wakati Waziri huyo alipotembelea soko hilo mkoani Pwani. Wa tatu kushoto ni Naibu Waziri Uchukuzi, Atupele Mwakibete.
Naibu Waziri wa Uchukuzi, Atupeleke Mwakibete, akizungumza na wazee wa Wilaya ya Chalinze wakati alipotembelea Wilaya hiyo, mkoani Pwani. Kulia kwa Naibu Waziri Mwakibete ni Naibu Waziri wa Ardhi na Maendeleo ya Makazi ambaye pia ni Mbunge wa Chalinze, Ridhiwani Kikwete.
No comments
Post a Comment