Wizara ya afya yaahidi mkakati endelevu kwa watoto waliofanyiwa upasuaji Muhimbili
Wizara ya afya imesema itaweka mkakati kuwafuatilia watoto Rehema na Neema waliofanyiwa upasuaji wa kutenganishwa katika hospitali ya taifa ya Mhimbili.
Hayo yamesemwa na Waziri wa afya Ummy Mwalimu, alipowatembelea watoto hao ambapo amesema Wizara itaweka mkakati endelevu wa kuwafuatilia Watoto hao kujua hali zao pamoja na kutoa msaada kwa familia huku akimpongeza Mama wa mapacha Rehema na Neema kwa ujasiri na kuweza kujifunga Watoto mapacha katika Hospitali ya Wilaya ya Maswa.
Waziri Ummy amefurahishwa na hali za
maendeleo ya kiafya ya Watoto hao kuendelea vizuri na kuwapongeza jopo la
Madaktari kutoka Hospitali ya Taifa Muhimbili pamoja na Madaktari kutoka Nchi
ya Falme ya Bahrain.
“Wataalamu wetu wamefanya upasuaji wa
kuwatenganisha kwa mafanikio makubwa, nimefurahi kuona Watoto wanaendela
vizuri, wamenieleza upasuaji huu ni mgumu sana, leo ni siku ya nne na Watoto
wanaendelea vizuri tunamshukuru Mungu” amesema Waziri Ummy Mwalimu
Waziri Ummy Mwalimu amesema katika
Mwaka huu mpya wa Bajeti 2022/23 Serikali imetenga kiasi cha Shilingi Bilioni 8
kwa ajili ya mafunzo kwa madaktari ili waweze kuongeza ujuzi na kuweza kutoa
huduma za kibingwa hapa nchini.
“Tunao wajibu wa kuweka rasimali fedha kwa ajili ya mafunzo kwa watumishi, vifaatiba pamoja na dawa na miundombinu, tutaendelea kuweka fedha kwa ajili ya mafunzo kwa madaktari bingwa na bingwa bobezi” amesema Waziri Ummy
No comments
Post a Comment