Waandishi wa Blogs na Online tv kufanya kazi kwa weledi na kufuata kanuni na sheria
Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA)
imewataka waandishi wa habari wa vyombo vya habari vya mitandao ya kijamii
ikiwemo Blogs na Youtube (Bloggers & Youtubers) kufanya kazi kwa weledi
wakizingatia Sheria na Kanuni zinazowaongoza.
Meneja wa Mamlaka hiyo Kanda ya Ziwa,
Mhandisi Francis Mihayo ametoa rai hiyo Julai 06, 2022 jijini Mwanza, wakati
akifungua kikao kazi baina ya TCRA na waandishi wa habari wa vyombo habari
mtandaoni kilicholenga kujengeana uelewa kuhusu mabadiliko madogo ya Kanuni za
maudhui mtandaoni.
Mhandisi Mihayo amesema baada ya sekta ya
habari mtandaoni kukua hapa nchini, zimeibuka changamoto mbalimbali ikiwemo
upotoshaji unaofanywa na baadhi ya runinga za mtandaoni ambapo kichwa cha
habari kinakuwa hakina mahusiano na maudhui yaliyo ndani ya habari.
“Unakuta kichwa cha habari kimeandikwa ‘Imeisha Hiyo’ ukiingia ndani unakuta mwanzo hadi mwisho mtangazaji anasema na neno ‘Subcribe, bonyeza kengele’ kwa habari zaidi, sasa hiyo kwa wataalamu wenye leseni kutoka TCRA sitegemei muwe na kitu kama hicho” amesema Mhandisi Mihayo.
Pia Mhandisi Mihayo amesema kuna baadhi ya makosa yamekuwa yanafanywa na vyombo vya habari kwa kujumuisha taasisi nzima pale mtumishi mmoja anapokuwa ametenda kosa lizilo la kimaadili jambo ambalo amesema si weledi.
“Mfano labda mimi ni mlevi na nimekamatwa huko mtaani nazurura, badala ya kusema Mhandisi Mihayo nimekamatwa, mnaandika TCRA yaendekeza ulevi, hiyo si sawa, mnatakiwa kudili na mimi bila kuingiza TCRA” amesisitiza Mhandisi Mihayo.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Chama cha Waandishi wa Habari Mkoa Mwanza, Edwin Soko akiwasilisha mada kuhusu usalama wa waandishi wa habari mtandaoni, amesema wanapaswa kuwa makini kwa kuimarisha ulinzi wa vifaa vyao mtandaoni ili kuepuka kudukuliwa kwani hiyo ni changamoto kubwa kwa sasa.
“Kuna mambo mbalimbali yanayoashiria vitisho
vya kimtandao ambayo mnatakiwa kuwa nayo makini ikiwemo kutoshawishiwa
kubonyesha ‘links’ zinazoshawishi kwamba umeshinda zawadi (phishing). Mwaka
2013/15 Facebook na Google walilipa dola milioni 100 kwa watu wasiowahusika
baada ya kudukuliwa kutokana na kubonyeza ‘links za aina hiyo” amesema Soko
huku akihimiza watumiaji wa mitandao ya kijamii kukinga vifaa vyao kwa kuweka
nywila (password) na programu za kupambana na wavamizi mtandaoni (Malware
Virus).
Akiwasilisha mada kuhusu maadili ya uandishi
wa habari, Mwenyekiti Mstaafu wa MPC Deus Bugaywa amesema changamoto iliyopo
kwenye vyombo vya mtandaoni ni kutopitia kwenye dawati la uhariri wa zaidi ya
mtu mmoja na hivyo kuwa na makosa mengi ya kimaadili ambapo wengi wa watoa
maudhui wamekuwa wakitaka kuwa wa kwanza kutoa maudhui mtandaoni.
Mamlaka ya TCRA Kanda ya Ziwa imetumia kikao
hicho kutoa ufafanuzi kwa waandishi wa habari mtandaoni kuhusiana na mabadiliko
madogo ya Kanuni za Maudhui Mtandao yaliyofanyika mwaka huu 2022 kwa lengo la
kuboresha Kanuzi za hapo awali zilizotoka kwa mara ya kwanza mwaka 2018 chini
ya Sheria ya EPOCA ya mwaka 2010.
Mabadiliko yaliyofanyika ni pamoja na kupuguza ada ya leseni kutoka shilingi milioni moja hadi shilingi laki tano kwa mwaka na ada ya maombi kutoka shilingi laki moja hadi shilingi elfu hamsini. Lakini pia waandaani wa maudhui yanayohusu michezo, sanaa, mapishi na elimu hawatahitaji kuwa na leseni kutoka TCRA bali leseni hiyo itatolewa kwa wale wanaotoa maudhui ya Habari (News and Current Affairs).
Akiwasilisha mada kuhusu Kanuni za
maudhui mtandaoni za mwaka 2022, Mwanasheria TCRA Joseph Kavishe
amesema ni kosa la jinai kuendesha mtandao wa kijamii bila kusajili hivyo
kuwasihi bloggers & youtubers kusajili blogs na Online Tv zao ili kuepuka
mkono wa sheria huku akiwataka kulinda utu wanapoandika habari zao wakitumia
lugha nzuri.
No comments
Post a Comment