Kundi la mataifa ishirini yaliyostawi zaidi kiviwanda duniani G-20 linakutana leo Ijumaa mjini Bali Indonesia, katika wakati ambapo Marekani inayashinikiza mataifa yenye uchumi mkubwa duniani kuiwekea vikwazo zaidi Urusi kutokana na uvamizi wake nchini Ukraine. Mkutano huo utawakutanisha wanadiplomasia wakuu wa Marekani na Urusi kwa mara kwanza tangu kuzuka kwa vita hivyo. 


Waziri wa mambo ya nje wa Marekani Antony Blinken anatarajiwa pia kufanya mazungumzo na mwenzake wa China Wang Yi, ikiwa ni mara ya kwanza baada ya miezi kadhaa kufuatia msuguano kati ya Beijing na Washington juu ya Taiwan. 


Blinken hata hivyo ataepuka mkutano wa moja kwa moja na waziri wa mambo ya nje wa Urusi Sergei Lavrov, na badala yake ameilaumu Moscow kwa kuchochea migogoro ya chakula na nishati duniani. Blinken amehimiza wanachama wa G-20 kuunga mkono mpango wa Umoja wa Mataifa wa kufungua tena bandari zilizofungwa kutokana na vita vinavyoendelea Ukraine.