Wavamia jela na silaha, waachia wafungwa
Watu wenye
silaha wametumia vilipuzi kulipua gereza karibu na mji mkuu wa Nigeria na
kuwaachia mamia ya wafungwa lakini wakuu wa magereza wamesema wamewakamata tena
wengi waliotoroka.
Wakazi katika eneo hilo
waliripoti kusikia milipuko na milio ya risasi Jumanne jioni karibu na Kituo
cha Ulinzi cha Kuje, nje kidogo ya Abuja, na vikosi vya usalama vilikuwa
vimelizingira eneo hilo mapema jana.
Ofisa mmoja wa usalama aliuawa
wakati watu hao wenye silaha walipovunja gereza hilo kwa kutumia vilipuzi,
msemaji wa idara ya marekebisho ya tabia za wafungwa, Abubakar Umar, alisema.
“Baadhi ya wanaume waliokuwa
kizuizini walitoroka. Tuliweza kuwakamata wengi wao asubuhi ya leo. Zaidi ya
300 walitoroka, lakini tumewakamata tena karibu 300,” aliwaambia waandishi wa
habari jana.
Alisema maofisa wa magereza bado
wanang’amua ni wangapi ambao hawajapatikana.
Kamanda mkuu wa polisi wa
zamanui, Abba Kyari, ambaye alikuwa anashikiliwa katika gereza la Kuje
akisubiri kufikishwa mahakamani kwa tuhuma za kusafirisha dawa za kulevya, bado
yuko kizuizini, alisema Umar.
“Tulisikia milio ya risasi mtaani
kwetu. Tulidhani ni majambazi wenye silaha,” mkazi mmoja wa eneo hilo alisema.
Haijabainika ni nani
aliyetekeleza shambulio hilo lakini vikosi vya usalama vya Nigeria vinapambana
na wanajihadi, magenge ya wahalifu wenye silaha nzito na wanamgambo wanaotaka
kujitenga katika maeneo tofauti ya nchi.
Mashambulizi dhidi ya magereza nchini Nigeria yametokea siku za nyuma, huku watu wenye silaha wakitaka kuwaachilia wafungwa.
Zaidi ya wafungwa 1,800 walitoroka mwaka jana baada ya watu waliokuwa na silaha nzito kushambulia gereza moja kusini magharibi mwa Nigeria kwa kutumia vilipuzi.
Washambuliaji hao waliipbuka
katika gereza la Owerri katika jimbo la Imo, wakikabiliana na walinzi kwa
risasi kabla ya kuvamia gereza hilo.
Jimbo la Imo ni kitovu cha
makundi yanayotaka kujitenga yanayotafuta taifa huru kwa ajili ya wakazi wa
kiasili wa Igbo.
No comments
Post a Comment