Tanzania Yapokea Chanjo Ya Uviko-19 Aina Ya Sinopharm
Tanzania imepokea chanjo ya
UVIKO-19 aina ya Sinopharm dozi Milioni tatu (3,000,000) ambazo zitawasaidia
kuwakinga wananchi 1,500,000 dhidi ya maambukizi ya ugonjwa wa virusi vya
Korona.
Chanjo hizo zimepokelewa na Kaimu Mkurugenzi wa Kinga Dkt. Beatrice
Mutayoba wakati wa mapokezi ya chanjo hizo kwa niaba ya Serikali ya Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania jijini Dar es Salaam kutoka Jamhuri ya Watu wa China.
“Chanjo hizi zimetolewa kwa hisani ya mke wa Rais wa China Prof. Peng Liyuan,
kwa niaba ya Serikali yetu nitoe shukrani sana kwa Serikali ya China hususani
katika kujali Afya za watanzania kwa kutupatia chanjo hizi.” Amesema Dkt.
Beatrice
Amesema hadi kufikia Julai 12, 2022 jumla ya dozi 21,226,520
zimepokelewa kutoka shirika la COVAX pamoja na nchi wahisani na tayari
zimeshasambazwa katika maeneo yote nchini.
“Kuna Mikoa ambayo imezidi asilimia 30 ya utoaji wa huduma za chanjo
ikiwemo Dar es Salaam lakini pia kuna Mikoa ambayo haijazidi asilimia 20 hivyo
niwaombe mkaongeze juhudi za kutoa elimu kwa watanzania ili tuendelee kuwakinga
na UVIKO-19. ” Amesema Dkt Beatrice
Dkt. Beatrice amesema kuwa wagonjwa wanaolazwa kutokana na kupata
virusi vya Korona wengi wao wanakuwa hawajapata chanjo ya UVIKO-19 kutokana na
takwimu zilizofanywa na wizara ya Afya.
Aidha, amewasihi watanzania wote wenye umri kuanzia miaka 18 kama inavyoshauriwa
na wataalamu wa Afya kwenda kupata chanjo ya UVIKO-19 kwakuwa chanjo hiyo ni
salama na haina madhara na kuendelea kuchukua tahadhari zote za kinga dhidi ya
ugonjwa huo wa virusi vya Korona.
Kwa upande wake mwakilishi wa Balozi wa China Bw. Salim Chu Kun ametoa
pongezi kwa Serikali ya Tanzania kupitia wizara ya Afya kwa kuendelea kujali
Afya za watanzania wote hususani wakina mama na ameahidi kuendelea kuisaidia
Tanzania na mapambano dhidi ya UVIKO-19.
Naye,Mkurugenzi wa masuala ya jinsia na wanawake kutoka wizara ya
Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Bi. Grace Mwangwa
ameishukuru wizara ya Afya kwa kutambua uwepo wao na ameahidi kuendelea kutoa
ushirikiano katika masuala ya Afya kwa kuwa tunajenga nchi moja.
Serikali kupitia wizara ya Afya iliidhinisha matumizi ya chanjo aina ya
Janseen, Pfizer, Moderna, Sinopharm, Sinovac, na Covaxin baada ya kujiridhisha
na vigezo vya ubora, usalama na ufanisi kwa matumizi ya watanzania kuanzia umri
wa miaka 18 na kuendelea.
Katika mapokezi hayo yamehudhuriwa na viongozi mbalimbali kutoka wizara
ya Afya akiwepo Meneja mpango wa Taifa wa chanjo Dkt. Florian Tinuga na Mganga
mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Dkt. Rashid Mfaume
No comments
Post a Comment