Mahakama kuu kanda ya Iringa iliyokaa kikao chake katika mahakama ya hakimu mkazi mkoa wa Njombe imewahukumu washtakiwa watatu Elias Jackson Mwenda (31) , Hussein Khamis (31) na Orestus Mbawala(51)kunyongwa hadi kufa baada ya kukutwa na hatia ya mauaji ya James Kaengesa mkazi wa Makambako mkoani Njombe.


Akisoma hukumu hiyo  jaji Dk. John Utamwa amesema tukio hilo la mauaji lilitokea mtaa wa Mashujaa uliopo halmashauri ya mji wa Makambako hapa mkoani Njombe.


Amesema tukio hilo lilitokea Juni mwaka 2016 mnamo saa mbili usiku ambapo marehemu ambaye  alikuwa dereva wa bodaboda  aliyokuwa akiimiliki alikodiwa na moja ya washtakiwa hao na alipofika eneo la Mashujaa aliambiwa asimame na mshtakiwa huyo ambaye alikuwa amepakiwa kwenye bodaboda hiyo.


Jaji Utamwa amesema eneo ambalo marehemu alisimamisha bodaboda yake  kumbe  ndipo ambapo washtakiwa  walikubaliana endapo mwenzao atakodi bodaboda mpya asimame eneo hilo.


"Ndipo walimkaba marehemu na kumnyonga kwa kutumia kamba ambayo waliitengeneza mkoani Njombe na kupora pikipiki" amesema Dk. Utamwa.


Baada ya kumyonga marehemu na kumuua amesema washtakiwa hao walimtupa kwenye shamba la mahindi na kutoweka na pikipiki kuelekea mkoani Mbeya ambapo walikamatwa eneo la Rujewa wakiwa na pikipiki hiyo.


Amesema hukumu hiyo kwa washtakiwa hao imetolewa kutokana na wao kwenda kinyume cha sheria chini ya kifungu cha 196 na 197 cha kanuni ya adhabu sura ya 16 marejeo ya mwaka 2019.


Mawakili wa serikali ambao walikuwa upande wa jamhuri na kuwakilishwa na Matiku Nyangero na Andrew Mandwa wameiomba mahakama kutoa adhabu kwa mujibu wa kifungu cha 197 cha kanuni ya adhabu sura ya 16 marejeo ya 2019 kwakuwa adhabu ya mauaji ya kukusudia ni moja tu ya kunyongwa hadi kufa.


"Pikipiki iliyokuwa kielelezo cha sita upande wa jamhuri iliyokuwa mali ya marehemu arudishiwe mke wa marehemu ambaye anaitwa Enelika Nyenzi" amesema Nyangero.


Mawakili upande wa utetezi ambao uliwakilishwa na Musa Mhagama,Byton Kaguo na Octavian Mbungani wamelkubaliana na maombi yaliyotolewa na mawakili upande wa serikali.